Tuesday, March 18, 2008

Muungano nje ya Tip Top!



Katika hali ambayo naweza kuiita ya kushangaza...wale wasanii wawili maswahiba......Mb Dogg na mwenzake Deso, ambao sio siku nyingi zilizopita walijitoa kwenye kundi lao la zamani la...'Tip Top Connection' wameungana na kuunda umoja wao Chini ya jina la 'Wamanza Bay'.
Kwa mujibu wa wawili hao....lengo la muungano huo ni kusaidiana katika kazi zao za sanaa kama familia na wala sio kama kundi.

``Tumekuwa na mahusiano mazuri tangu tukiwa ndani ya kundi letu la zamani....tumeona iko haja ya kukaa pamoja na kushirikiana.....ni ushirikiano wa kupeana kampani katika mambo mengi ya kikazi,`` alisema Deso.

``Kila msanii anaweza kuendelea kufanya kazi zake kivyake na kutoa albam zake lakini, unafanya hivyo huku ukijua una mtu ama watu wa familia yako wanaokusapoti.....ndio maana nzima ya familia yetu hii,`` alisema Deso.

Hivi sasa kundi hilo linajiandaa kupiga picha za pamoja kwa ajili ya kuutangaza muunganiko wao...na wana imani mambo yakienda kama yalivyopangwa watafanya familia kubwa zaidi na kuibua vipaji vya wasanii wengi waliofichika.

Tuzo za vinara wa Filamu kusheheni Mei 2008



Baada ya kufana kwa uzinduzi wa Tuzo za Vinara wa filamu Tanzania, na waandaaji wanaalikwa kujaza fomu za ushiriki ili kuweza kuwasilisha kazi zao katika Tuzo za 2008.
Fomu hizi zitapatikana ndani ya ofisi za BASATA (Muulizie Omar Mayanga), Wananchi Wote, Kapico, GMC na Game First Quality.

Baada ya kujaza fomu watengezaji wa filamu wanatakiwa kurudisha fomu na nakala ya kazi kwenye ofisi za BASATA kwa Omar Mayanga.

Pia utoaji tuzo za Vinara wa Filamu Tanzania unalenga katika kuifanya sanaa ya Tanzania kupata nguvu mpya na kuwafanya watengenezaji na wadau wa sanaa kufanya bidii katika ushindani wa soko la sanaa.

Wameamua kufanya hivyo ili kutengeneza kazi zilizo bora zaidi zinazoweza kuuzika kimataifa, ili nchi yetu iwe katika ramani ya dunia.

Tuzo za Vinara wa Filamu Tanzania pia zinalenga kuwafanya wananchi kuendelea kuwa na mwamko wa kupenda kaz, zinazotengenezwa na Watanzania wenzao ili kupata mafunzo mbalimbali yatokanayo na kazi za wasanii na pia kukuza soko kwa faida ya pande zote mbili.

Katika fomu hizo, kutaainishwa mambo muhimu ambayo mtengenezaji wa filamu atapaswa kujaza.

Fomu hiyo itakuwa na maswali mengine yaani filamu imetengenezwa lini, mahali ilikotengenezwa, maudhui ya filamu na lugha iliyotumika.

Baada ya fomu hizo kujazwa kwa usahihi, zitatumwa kwenye ofisi za waandaji, kwa mkono au njia ya posta kwa anuani kamili ya waandaji. Watengenezaji wa filamu husika watapaswa kuambatanisha na mkanda wa filamu (VHS/DVD/VCD).

Kutakuwa na jopo la majaji wanane (8) watakaochaguliwa na waandaji kwa kushirikiana na Baraza la sanaa la Taifa nchini, watakaokuwa na jukumu la kupitia filamu zote na kuzitolea uamuzi.

Majina na wasifu za majaji zitawekwa bayana hivi karibuni, pia vigezo zitakazotumika zitawekwa wazi.

Filamu zitakazoingizwa kuwania tuzo ni zile zilizotengenezwa na Watanzania kuanzia Januari 2007 hadi mwisho wa siku ya kualikwa watengenezaji kuingiza filamu zao ambayo itakuwa 31 Machi 2008.

Kushiriki kwa watengezaji wa filamu itasaidia kupata Filamu Bora ya Mwaka, Muigizaji Bora wa Mwaka wa Kiume, Muigizaji Bora wa Mwaka wa Kike, Muigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Kiume, Muigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Kike, Mwongozaji Sinema Bora wa Mwaka, Mchekeshaji Bora wa Mwaka, Mwandishi Bora wa Filamu, Mtunzi Bora wa Filamu, Filamu Bora ya kutisha, Muigizaji Mwandamizii Bora wa kike (supporting actor), Muigizaji Bora Mwandamizi wa Kike; Adui Bora kwenye Filamu, Mhariri Bora wa Filamu na mapambo na maleba ya mwaka.

Pia itatolewa tuzo ya heshima kwa wale waliotoa machango wao kukuza sanaa ya hapa nchini.

Tukio la utoaji wa tuzo hizi limepangwa kufanyika mwezi Mei 2008 na litafanyika kila mwaka.